AJIRA MPYA ZA WALIMU (UALIMU) MWAKA 2013/14 KAMA YALIVYOTOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU NA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI)
- Walimu shule ya msingi - Cheti
- Walimu Sekondari - Stashahada(Diploma)
- Walimu Sekondari - Shahada (Degree)
- Wakufunzi/Walimu wa vyuo/shule za mazoezi.
***********************&*********************
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA
MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU
YA AJIRA KWA
WALIMU WAPYA MWAKA 2013/14
Jumla ya Walimu wapya 36,021
ambao wamehitimu mwaka 2013 kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini wataajiriwa
rasmi na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri) ifikapo tarehe 01 Aprili
2014. Kati ya idadi hiyo walimu wa ngazi ya Cheti (Daraja III A) ambao
hufundisha katika shule za Msingi ni 17,928 na walimu wa shule za sekondari ni
18,093 (wakiwemo 5,416 wa Stashahada na 12,677 wenye shahada).
Orodha rasmi ya walimu wapya
ikionesha Halmashauri mbalimbali walikopangwa itatangazwa kwenye
tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI
(www.pmoralg.go.tz) na ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi (www.moe.go.tz) ifikapo
tarehe 15 Machi, 2014.
Walimu wote wapya wanatakiwa
kuripoti bila kukosa kwenye Halmashauri walikopangiwa ifikapo tarehe 01 Aprili,
2014 ili waanze kazi mara moja. Inasisitizwa kwamba walimu waripoti tarehe hiyo
ili
taarifa zao za kiutumishi
zifanyiwe kazi na Waajiri wao yaani Wakurugenzi ili kuwawezesha kupata mshahara
mwezi Aprili 2014 na hivyo kuepuka ulimbikizaji wa mshahara kwa watumishi wapya
wanaoanza ajira.
Mwalimu yoyote ambaye ataripoti
baada ya tarehe 10 Aprili, 2014 bila sababu za msingi zinazokubalika kiutumishi
atakuwa amepoteza nafasi hiyo.
Ikumbukwe kwamba Upangaji wa
Walimu wapya kwenye Halmashauri umezingatia uwepo wa mahitaji ya walimu. Vile vile,
fedha za kujikimu kwa muda wa siku saba na nauli ambazo zitalipwa kwa kila
mwalimu atakayeripoti kulingana na viwango vilivyowekwa na Serikali zimetumwa kwenye
Halmashauri walikopangwa walimu hao. Hivyo, kila mwalimu anatakiwa kwenda
kuripoti katika Halmashauri alikopangwa.
Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI
haitafanya mabadiliko yoyote ya vituo vya kufanya kazi walimu wapya isipokuwa
kwa utaratibu wa kawaida wa uhamisho baada ya mwalimu kutimiza vigezo na
masharti ya uhamisho.
Ni vema ifahamike kuwa ajira
zinazotangazwa ni za walimu wapya.Walimu ambao tayari ni watumishi umma
waliokuwa vyuoni kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na hivi sasa wamehitimu
mafunzo yao,wanatakiwa kurudi kwa waajiri wao na kuendelea na kazi.
IMETOLEWA NA
JUMANNE A. SAGINI
KATIBU MKUU
OFISI YA WAZIRI MKUU - TAMISEMI